UUNGU UPO NDANI YAKO, USIUTAFUTE NJE YAKO

You are currently viewing UUNGU UPO NDANI YAKO, USIUTAFUTE NJE YAKO


Katika nyanja mbalimbali za maisha ya kiroho na kifalsafa, kumekuwa na tafakari nyingi juu ya mahali pa kuutafuta Uungu. Wengi hutumia muda mwingi wakitafuta uwepo wa Uungu katika vitu vya nje kama vile makanisa, misikiti, au hata maeneo matakatifu, wakiamini kuwa ukaribu na sehemu hizi unawaleta karibu na nguvu ya uumbaji (Uungu) Muumba. Hata hivyo, mtu hapaswi kumtafuta Mungu nje ya nafsi yake, bali anapaswa kuelekeza mawazo na tafakari ndani yake ili kugundua uwepo wa kiungu unaokaa ndani ya kila mtu.

KUMBUKA: Neno Mungu linavalisha uhusika wa kitu au kiumbe kwa muumbaji, lakini muumbaji sio kitu wala sio mtu wala sio kiumbe. Muumbaji anasimama kama quality iliopo ndani ya kila kitu kinachoonekana na kisichoonekana. Kilichopo hai na kisicho hai. Hivyo Imenilazimu kutumia neno linalobeba uwepo wake kwa kila kitu ambalo ni UUNGU. Uungu halisimamj kama jina bali linasimama kama kiwakilishi kilichobeba uwepo wa hali ya ubora wa kiungu ndani ya kilakitu.

ASILI YA UUNGU NDANI YA MWANADAMU NI NINI?

Katika maandiko mengi ya kidini na mafundisho ya kiroho, kuna msisitizo mkubwa kuwa mwanadamu aliumbwa kwa mfano na sura ya Mungu. Kwa mfano, katika Biblia (Mwanzo 1:27) imeandikwa, “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba.” Hii inaashiria kwamba ndani ya kila binadamu kuna chembe ya uungu inayompa uwezo wa kufikiri, kupenda, kusamehe, na kuumba. Katika Uislamu, kuna dhana ya fitra, inayoeleza kuwa kila mwanadamu huzaliwa na maarifa ya ndani ya uwepo wa Uungu. Mafundisho ya Kihindu kupitia Upanishads yanasisitiza kuwa Atman (nafsi ya ndani) ni sawa na Brahman (Uungu mkuu), ikimaanisha kuwa Uungu upo ndani ya kila mtu.

HAPA NDIPO INAINGIA TAHAJUDI

Picha hii huonyesha mfano wa mtu anapokuwa anafanya tahajudi.

Tunahimizwa kufanya tafakari ya ndani badala ya kutegemea vitu vya nje kukuleta karibu na Uungu. Njia kama meditation (kutafakari) na maombi ya kimya husaidia watu kuungana na sehemu ya kiuungu iliyo ndani yao. Kwa mfano, katika Injili ya Luka 17:21, Yesu anasema, “Ufalme wa Mungu umo ndani yenu,” akimaanisha kuwa mtu hahitaji kwenda mahali fulani ili kuukuta Uungu, bali anapaswa kujiangalia ndani yake mwenyewe.

Kwa mtazamo wa kiroho, tunaponyamaza na kuelekeza mawazo yetu ndani, tunagundua hali ya amani, upendo, na mwanga wa kiuungu ambao hauhitaji uthibitisho wa nje. Mafundisho ya Wabuddha yanasisitiza kuwa mtu akiamka kiroho (enlightenment), anagundua kuwa amebeba ukweli wote ndani yake na hakuna cha kutafuta nje.

UDANGANYIFU WA KUUTAFUTA UUNGU NJE YETU!!

Picha hii ikionyesha kufungwa kwa akili kwakuambiwa uongo unaoshawishi.

Mara nyingi wanadamu hudhani kuwa ukaribu na Uungu (Asili) unapatikana kwa njia za nje kama kwenda maeneo matakatifu, kufuata ibada kwa mazoea, au kupata baraka kutoka kwa wengine. Ingawa haya yanaweza kusaidia katika kuimarisha imani, kuna hatari ya kupoteza uelewa kwamba uwepo wa Uungu ni wa ndani na si wa nje. Mwanadamu anapoutafuta Uungu nje, anaweza kujikuta akizama katika ibada ya kipepo ya nje bila kuwa na mabadiliko ya ndani. Ukweli ni kwamba bila safari ya ndani ya kujitambua, mtu anaweza kupoteza uhusiano wa moja kwa moja na asili yake ya kiuungu.

KUNA FAIDA GANI KATIKA KUNTAMBUA UUNGU NDANI YAKO??

Uhuru wa kiroho – Mwanadamu anapogundua kuwa Uungu upo ndani yake, hawezi kudanganywa au kupelekwa pelekwa tu na upepo wa nje. Anaishi kwa uhuru wa ndani na utulivu wa nafsi.

Amani ya ndani – Kujua kuwa Uungu upo ndani ya nafsi huleta amani ya kudumu, kwa sababu mtu hahitaji kusafiri au kutegemea vitu vya nje kupata amani hiyo.

Nguvu ya kubadilisha maisha – Mwanadamu anapogundua nguvu ya kimungu ndani yake, anaweza kushinda changamoto na kuishi kwa ujasiri na matumaini.

Upendo na Huruma – Kutambua uwepo wa Uungu ndani hufanya mtu awe na upendo kwa wengine, kwa sababu anaelewa kuwa kila mtu ni mwakilishi wa uungu huo.

Kauli hii “Mungu yupo ndani yako, usimtafute nje yako” ni mwaliko wa kufanya safari ya ndani ya kujitambua na kugundua uwepo wa kimungu unaoishi ndani ya kila mmoja wetu. Badala ya kupoteza muda na nguvu tukimtafuta Mungu katika vitu vya nje, tunapaswa kuelekeza mawazo yetu ndani ya nafsi na kugundua ukweli wa kina: kwamba Uungu upo nasi daima, ndani yetu, ukisubiri tuutambue na kuungana nao kwa ukamilifu. Safari ya kweli ya kiroho si kutoka nje kwenda mbali, bali ni safari ya kurudi ndani ya nafsi zetu ambapo Uungu umekuwa daima.

Ikiwa umesoma na kufikia hapa nikupongeze sana lakini nikuhamasishe ujitahidi kuungana na nguvu ya Uungu iliyopo ndani yako.

🙏Amani, Furaha na Rehema zikakujaze. 🙏

🌹Nakuoenda sana na ikikupendeza jaribu ku share na wale uwapendao ili kuwapa chakula cha kiroho.🌹

Leave a Reply